1.    UTANGULIZI

Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (39th Ordinary Summit of SADC Heads of State and Government– SADC) ulifanyika Dar es Salaam, Tanzania tarehe 17 na 18 Agosti, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (        JNICC). Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ifuatayo: -

i.              Tarehe 9-11 Agosti, 2019:     Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu (Meeting of the Standing Commitee of Senior   Officials);

ii.            Tarehe 13- 14 Agosti, 2019:   Mkutano wa Mawaziri (Council of Ministers  Meeting);

iii.           Tarehe 16 Agosti, 2019:         Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Zambia Mwenyekiti wa sasa, Angola Mwenyekiti aliyemaliza muda   wake, na Zimbabwe Mwenyekiti anayeingia);

Aidha, mkutano huo ulitanguliwa na matukio yafuatayo:-

i.              Tarehe 5 hadi 9 Agosti, 2019         Maadhimisho ya Awamu ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC yaliyofanyika, JNICC, Dar es Salaam.

ii.            Tarehe 15 Agosti, 2019                   Mhadhara wa Umma kuhusu SADC

(Public Lecture) uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

2.    MUUNDO WA MKUTANO

Ajenda zote za Mkutano zilijadiliwa kwanza katika ngazi ya Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ambayo ilitoa mapendekezo kwa ajili ya Baraza la Mawaziri. Baraza hilo lilijadili ajenda hizo na mapendekezo yaliyotolewa na Makatibu Wakuu na kuyafanyia maamuzi. Baadhi ya masuala yaliamuliwa kwa ajili ya utekelezaji katika ngazi ya Baraza la Mawaziri na masuala mengine muhimu yaliainishwa kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC. Orodha ya masuala muhimu yatakayojadiliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali yamefafanuliwa kwa kina katika taarifa hii.

3.    MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI KATIKA MKUTANO HUU

3.1 Kutoa tuzo kwa washindi wa mashindano ya SADC

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Hage Gengob, Rais wa Jamhuri ya Namibia na Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake alitoa zawadi kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari walioshinda tuzo za mashindano ya uandishi wa Insha ya SADC pamoja na kutoa zawadi kwa waandishi wa Habari walioshinda Tuzo za Habari za SADC kwa mwaka 2019.

 Katika mashindano ya Insha ya SADC, mshindi wa kwanza alitoka Jamhuri ya Botswana; mshindi wa pili alitoka Jamhuri ya Zimbabwe na mshindi wa tatu alitoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa upande wa Tanzania wanafunzi walioshinda katika uandishi wa insha, mshindi wa kwanza ni Cynthia Masuka kutoka Shule ya Sekondari Longido (Arusha), mshindi wa pili ni Ruvina Daudi Warimba kutoka Shule ya Sekondari ya Morogoro na mshinidi wa tatu ni   Julieth Mpuya kutoka Shule ya Sekondari Kilangalanga (Pwani). Aidha, Bi. Ruvina Daudi Warimba alishika nafasi ya tatu katika mashindano ya kikanda.

4.    AJENDA ZA MKUTANO

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ulipokea na kujadili ajenda kuu zifuatazo:-

1.    Uchaguzi wa Wenyeviti wa SADC na Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama.

2.    Hali ya Michango Kutoka Nchi Wanachama.

3.    Taarifa ya Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama Anayemaliza Muda Wake.

3.1 Kupitia taarifa ya hali ya ulinzi na usalama katika kanda.

3.2 Kupokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya SADC kuhusu Falme ya Lesotho.

3.3. Hali ya ulinzi na usalama nchini DRC.

3.4 Kuimarisha demokrasia katika kanda.

      i. Zimbabwe

      ii. Eswatini

iii.           Madagascar

iv.           DRC

v.            Afrika Kusini

vi.           Malawi

3.5 Chaguzi ndani ya kanda kuanzia tarehe 01 Agosti, 2019 hadi 31 Desemba, 2020.

3.6 Taarifa ya maendeleo kuhusu ujenzi wa bohari ya Jeshi la Akiba la SADC.

3.7 Tishio la ugaidi ndani ya kanda.

3.8 Taarifa ya hatua iliyofikiwa katika kuimarisha amani na utulivu, ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha demokrasia ndani ya kanda.

4.    Taarifa ya Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake.

5.    Taarifa ya Hali ya Uchumi ya SADC.

6.    Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe.

7.    Athari za Mabadliko ya Tabia Nchi na Jitihada za Kikanda.

8.    Jinsia na Maendeleo.

9.    VVU na UKIMWI.

10. Taarifa ya utekelezaji wa Kaulimbiu ya Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.

11. Uwasilishaji wa Kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.

12. Hali ya Utekelezaji wa Mkakati wa Viwanda na Mpango-kazi wake.

13. Mwongozo wa SADC wa ukusanyaji wa rasilimali.

14. Uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Uhawilishaji cha SADC (Virtual University Of Transformation).

15. Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya SADC.

16. Taarifa ya tathmini ya Burundi kukidhi vigezo vya kujiunga na SADC.

17. Taarifa ya Kongamano la Mshikamano wa SADC na Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi Magharibi (SADR).

18. Kubadilishwa kwa Jukwaa la Wabunge wa SADC kuwa Bunge la SADC.

19. Kuiunga mkono Zimbabwe kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.

20. Kupitia mikataba ya kisheria na masuala mengine ya kisheria.

21. Mengineyo.

22. Nchi Mwenyeji na Tarehe ya Kufanyika kwa Mkutano Ujao.

23. Taarifa kwa Umma (Communiqué).

5.    KUPOKEA UENYEKITI WA SADC

Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Mheshimiwa Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia, katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali iliyofanyika tarehe 17 Agosti, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC). Baada ya kukabidhiwa Uenyekiti, Mheshimiwa Rais alikaribishwa kutoa hotuba ya kupokea Uenyekiti (Acceptance Speech).

Baada ya ufunguzi, Mheshimiwa Rais alianza kwa kuongoza majadiliano katika kikao cha ndani cha Wakuu wa Nchi na Serikali (closed session) akishirikiana na Dkt. Stergomena L. Tax, Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC.

Mkutano huo ulimchagua Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama, na Mheshimiwa Dkt. Mokgweetsi E.K. Masisi, Rais wa Jamhuri ya Botswana kuwa Mwenyekiti Ajaye wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama.

Pia Mkutano huo ulichagua Makamu Mwenyekiti wa SADC Mhe. Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji ambaye anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2020 hadi Agosti, 2021. Uchaguzi huo hufuata ratiba ya mzunguko ambapo nchi ambazo hazijashika nafasi ya Uenyekiti kwa kipindi kirefu zitaorodheshwa na nchi mojawapo kuchaguliwa.

6.    HALI YA MICHANGO

Katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC uliofanyika mwezi Machi, 2019 mjini Windhoek, Namibia, pamoja na mambo mengine,  liliidhinisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020 ya SADC inayotokana na michango ya Nchi Wanachama ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 44,404.

Kwa mwaka 2019/2020, Tanzania ilitakiwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani 3,562,470. Tanzania imekamilisha malipo ya mchango wake kwa mwaka wa Fedha 2019/20. Aidha, Nchi Wanachama ambazo bado hazijawasilisha michango yao (Jamhuri ya Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) ziliombwa kuwasilisha michango hiyo kulingana na utaratibu uliowekwa.

7.    Taarifa ya Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama Aliyemaliza Muda Wake.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa Asasi ya Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama ulifanyika tarehe 16 Agosti, 2019. Mkutano huo uliongozwa na Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Zambia. Wajumbe wengine wa Mkutano huo walikuwa ni Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais wa Angola na Mwenyekiti wa SADC Organ aliyemaliza muda wake na Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe na mwenyekiti wa SADC Organ ajaye.

Kufuatia Mkutano wa Utatu wa Asasi hiyo (Organ Troika) ambao ulifanyika tarehe 16 Agosti, 2019, Mhe. Edgar Lungu, Mwenyekiti Anayemaliza muda wake aliwasilisha taarifa ya hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulikaofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2019.

Mkutano huo ulijadili taarifa hiyo kuhusu hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda, pamoja na taarifa muhimu zifuatazo:

·         Taarifa ya maendeleo ya utekelezaji ya maamuzi ya SADC katika Falme ya Lesotho;

·         Hali ya siasa na ulinzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC);

·         Uimarishaji wa demokrasia katika Kanda hususan katika nchi za Zimbabwe, Eswatini, Madagascar, DRC, Afrika Kusini na Malawi; na,

·         Taarifa za chaguzi zilizofanyika na zitakazofanyika katika kipindi cha tarehe 1 Agosti, 2019 hadi tarehe 31 Desemba, 2020.

Aidha, pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilijumuisha pia taarifa ya maendeleo kuhusu ujenzi wa bohari ya jeshi la akiba la SADC (SADC Standby Force Regional Logistic Depot); matishio ya kigaidi katika Kanda na taarifa kuhusu maendeleo ya jumla katika kuimarisha ulinzi na amani pamoja na uimarishwaji wa demokrasia ndani ya Kanda.

Katika mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali walipokea taarifa mbalimbali kuhusu masuala yaliyoorodheshwa kama ifuatavyo:-

Ø  Kuhusu Lesotho; Wadau wanaosimamia suala hili waliombwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa mabadiliko pamoja na kuridhia SADC kupeleka timu ya upatanishi na kuzuia migogoro kwa lengo la kuboresha jitihada zinazoendelea kufanywa na Msuluhishi wa SADC nchini Lesotho.

Ø  Kuhusu DRC; Nchi Wanachama waliwasilisha michango ya mawazo kwa ajili ya kuboresha taarifa ya ushauri ya ukamilishaji wa misheni ya DRC ifikapo mwisho wa mwezi Agosti, 2019. Aidha, pia Nchi Wanachama walitaka kushirikishwa katika kupitia na kutolea maoni mkakati wa Misheni ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC (MONUSCO) ambayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba 2019.

Ø  Kuhusu uimarishaji wa demokrasia katika kanda: Mkutano ulizipongeza nchi ambazo zimefanya uchaguzi kuanzia mwezi Agosti, 2018 hadi Julai, 2019. Nchi hizo ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Falme ya Eswatini, Madagascar, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe na Visiwa vya Komoro.

Ø  Kuhusu ujenzi wa bohari ya jeshi la akiba la SADC: Mkutano ulimpongeza Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambia kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika kufanikisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa kituohicho.

Ø  Tishio la Ugaidi: Mkutano huo uliziasa Nchi Wanachama kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kupambana na Ugaidi na mpango kazi wake, ikiwemo kuridhia kuunda taasisi ambayo itahusika na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia kwa wakati.

8.    Taarifa ya Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake

Mkutano huu ulipokea taarifa ya Mhe. Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake. Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilielezea masuala muhimu yaliyojiri wakati wa uenyekiti wake, ikiwemo majanga yaliyotokea katika kanda yakiwemo vimbunga kati ya mwezi Januari na Aprili, 2019 na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC.

Mkutano huo ulipokea taarifa hiyo na kumpongeza Mhe. Geingob kwa uongozi wake mahiri.

9.    TAARIFA YA HALI YA KIUCHUMI YA SADC

Katika Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walipokea taarifa ya hali ya Kiuchumi katika kanda kwa mwaka 2019/2020. Taarifa hiyo ilionesha ukuaji wa uchumi wa Kanda kwa asilimia 2.3 na kufanya vizuri katika kupunguza matumizi ambapo kwa mwaka 2019/2020 wastani wa asilimia 3.3 ya upotevu wa mapato ya ndani yaliokolewa.  Hali kadhalika, mfumuko wa bei ndani ya kanda umeongezeka kwa mwaka 2019 kutoka wastani wa asilimia 8 mwaka 2018 hadi wastani wa asilimia 11.1. Ongezeko hilo limetokana na kupungua kwa mvua kwenye maeneo mbalimbali ndani ya kanda pamoja na kujitokeza kwa majanga mengine kama vile vimbunga vya Cyclone, Desmond, Tropical Cyclone (Idai) and Cyclone Enawo yaliyoikumba Jumuiya kwa mwaka 2019.

10. HALI YA USALAMA WA CHAKULA NA LISHE

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ulipokea taarifa kuhusu hali ya usalama wa chakula katika Kanda ambayo ilionesha kutetereka kwa kiasi kikubwa katika mwaka 2019 ikilinganisha na mwaka 2018. Hali hii ilisababishwa na athari mbalimbali za hali ya hewa ikiwemo, Ukame katika upande wa Magharibi wa Ukanda, Mvua zilizokithiri, mafuriko na vimbunga vya IDAI na Keneth pamoja na wadudu waharibufu wa mazao na magonjwa. Hali hii imepelekea kupanda kwa bei za vyakula zikiambatana na changamoto za kiuchumi ndani ya Kanda.

      Aidha, madhara haya yameshabaisha uzalishaji wa nafaka (Mahindi, Mtama, mpunga, ngano na ulezi) ndani ya Kanda kupungua kwa asilimia 14 kutoka tani milioni 42.6mwaka 2018  hadi tani milioni 36.8 mwaka 2019. Hata hivyo, Tanzania na Afrika Kusini kwa kipindi hicho zilizalisha ziada ya mazao (surpluses) hayo ambayo yatakidhi kwa mwaka 2019/2020. Kutokana na hali hiyo, Tanzania ilitoa pole kwa Nchi zilizoathirika na majanga hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana katika masuala ya majanga. Aidha, Tanzania iliunga mkono programu mbalimbali za uwekezaji za kitaifa za kikanda zenye lengo la kuongeza uzalishaji wa kilimo katika ukanda na kuboresha biashara na maisha ya wananchi wa vijijini.

11.     MADHARA YA MABADILIKO YA TABIA NCHI NA JITIHADA ZA KIKANDA

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ulitaarifiwa kuhusu Mabadiliko yaliyokithiri ya tabia nchi na hali ya mvua zisizotabirika kwenye kanda ikiwa ni pamoja na hali ya ukame na mafuriko ambayo yamezikumba baadhi ya nchi ndani ya SADC na kusababisha madhara makubwa kwa baadhi ya nchi ikiwemo Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Madagascar.Hatua zilizochukuliwa na kanda katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ni kuiagiza Sekretarieti ya SADC kufanya utafiti wa mifumo ya kukabiliana na maafa iliyopo kwenye kanda ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho. Aidha, mkutano uliielekeza Sekretarieti ya SADC iongeze kasi ya maandalizi ya Mfuko wa Kanda wa Kukabiliana na Maafa na kuridhia kurejeshwa kwa Kamati ya Mawaziri ya Kukabiliana na Maafa ambayo itatakiwa kukutana kabla ya mwezi Machi, 2020;

12.     JINSIA NA MAENDELEO

Mkutano ulipokea taarifa ya utekelezaji wa Itifaki ya Jinsia ya SADC. Pamoja na mambo mengine, Itifaki hiyo inazitaka Nchi Wanachama wa SADC kuweka uwiano wa kijinsia kwa kuhakikisha kwamba wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na kupata nafasi za uongozi. Nchi Wanachama zinatakiwa kutoa taarifa za utekelezaji wa Itifaki hiyo kila mwaka zikiainisha takwimu za idadi ya wanawake Wabunge, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wakurugenzi Wakuu na Naibu Wakurungezi Wakuu.

Aidha, mkutano ulipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kanda wa Kuwezesha Wanawake na programu ya SADC ya ufuatiliaji wa Masuala ya Maendeleo ya Jinsia (Regional Multi-Dimensional Women Economic Empowerment Programme and 2018 SADC Gender and Development Monitor).

Katika kuhakikisha inatekeleza kwa Vitendo Azimio la SADC la Jinsia na Maendeleo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa Sera mbalimbali zinazosimamia utekelezaji wake ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Maendeleo ya Jinsia ya mwaka 2000, Sera ya Mashirika yasiyo ya kiserikali ya mwaka 2002 na Sera ya Wazee ya mwaka 2003 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar Sera ya Jinsia 2016, Sera ya Watoto 2001, Sera ya Hifadhi ya Jamii 2004, Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi 2019.

13.     UTEKELEZAJI WA KAULIMBIU YA MKUTANO WA 38 WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA SADC

Mkutano utapokea taarifa ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC iliyosema “Wekeza kwenye Miundombinu na Uwezeshaji Vijana kwa Maendeleo Endelevu”. Taarifa hiyo inaelezea hatua ambazo Serikali ya Namibia kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC imechukua katika kutekeleza kaulimbiu hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kuandaa rasimu ya mfumo wa kuwezesha vijana kushiriki kwenye shughuli za uvumbuzi, ujasiliamali, uongozi na kushiriki masuala ya SADC (Conceptual Framework on Promoting Youth, Innovation, Entrepreneurship, Leadership and Participation in SADC).

Aidha, mkutano uliipongeza Jamhuri ya Namibia, na kuielekeza Sekretarieti ya SADC kukamilisha maandalizi ya Programu ya kuendeleza vijana katika SADC (SADC Youth Development Programme) pamoja na kuhakikisha kwamba masuala ya vijana yanapewa kipaumbele katika Mpango Elekezi wa Maendeleo wa SADC kwa mwaka 2015-2020 (Revised RISDP 2015-2020).

14.     UWASILISHWAJI WA KAULIMBIU KUTANGAZA KAULIMBIU YA MKUTANO WA 39 WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA SADC

Wakuu wa Nchi na Serikali walipokea taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Rais na Mwenyekiti wa sasa wa SADC kuhusu Kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa mwaka 2019  ambayo ni  “Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC”. Kaulimbiu hiyo iliwasilishwa na Sekretarieti ya SADC na kuelezea  jinsi ambavyo imepanga mikakati ya kutekeleza kaulimbiu hiyo.

Wakuu wa Nchi na Serikali waliridhia kaulimbiu hiyo na kuiagiza Sekretarieti ya SADC kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa ya utekelezaji wake katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali mwaka 2020.              

15. HALI YA UTEKELEZAJI  WA MKAKATI NA MPANGOKAZI WA VIWANDA

Mkutano huu ulipokea taarifa ya utekelezaji wa mkakati wa viwanda wa SADC. Mkakati huu unalenga kuziwezesha nchi za SADC kukuza viwanda kwa kushiriki katika mnyororo wa thamani ndani ya kanda. Kwa kuanzia mkakati huo unatoa kipaumbele katika kuendeleza viwanda vya Dawa za binadamu, kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo; mkakati wa kunufaika na madini; na kuongeza thamani kwenye bidhaa.

Taarifa hiyo ilionesha kwamba kati ya vipengele 58 vilivyoainishwa kwenye mkakati huo, vipengele 5 vimetekelezwa kikamilifu; vipengele 46 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na 7 havijaanza kutekelezwa.

Aidha, taarifa hiyo ilionesha hatua iliyofikiwa na nchi wanachama katika kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kukuza viwanda kwenye kanda kwa kuzingatia nguzo nne za mkakati huo. Nguzo hizo ni Sekta ya viwanda; kujenga uwezo wa ushindani; ushirikiano wa kikanda; na masuala mtambuka. Hatua zilizotekelezwa katika nguzo hizo ni kama ifuatavyo:

a)    Viwanda

                i.        Tathmini ya viashiria vya uchumi mpana ilifanyika ili kuhakikisha kwamba nchi za SADC zinakuwa na uchumi thabiti unaochochea maendeleo ya viwanda.

              ii.        Suala la viwanda limepewa kipaumbele katika makubaliano kati ya  Sekretarieti ya SADC, Benki ya AfDB, Umoja wa Ulaya na Serikali ya Urusi ambapo miradi mbalimbali yenye lengo la kuendeleza viwanda itatekelezwa;

                iii.        Itifaki ya Viwanda ya SADC imekamilika;

               iv.        Tathmini ya mnyororo wa thamani kwenye sekta za kimkakati imefanyika ili kuweza kuainisha sekta za kipaumbele katika kutekeleza mkakati wa viwanda. Maeneo yaliyofanyiwa tathmini ni usindikaji wa mazao ya kilimo, mnyororo wa thamani kwenye huduma; mnyororo wa thamani katika madini na mnyororo wa thamani kwenye dawa; na

                  v.        Sera ya Madini ya Kanda na mpango kazi wake (Regional Mining Vision and Action Plan) vimekamilika. Sera hii inatoa mwongozo wa usimamizi wa sekta ya madini kwenye kanda pamoja na kuainisha mnyororo wa thamani wa madini ili kuchochea viwanda vya kuongeza thamani za madini kwenye kanda.

Katika utekelezaji wa mkakati huo, Tanzania imeanza mchakato wa kufanya mapitio ya Sera ya Viwanda ya Tanzania ili pamoja na mambo mengine, iweze kuendana na Mkakati wa Viwanda wa SADC. Vilevile Tanzania imeshiriki kikamilifu katika kuandaa Sera ya Viwanda ya SADC pamoja na kuendelea kupata mafunzo na kujengeana uwezo katika maeneo ya vipaumbele hususan kuongeza thamani mazao ya kilimo. Aidha, Tanzania imekamilisha Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint on Regulatory Reforms For Improved Business Environment) pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji wake ambao umeanza kutelekezwa tarehe 1 Julai, 2019. Kwa kuanzia jumla ya kodi na tozo 54 zimeondolewa.

Katika mkutano huu, Wakuu wa Nchi na Serikali walisisitizwa juu ya masuala yafuatayo:

i.             Nchi Wanachama kuhimizwa kutekeleza Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC;

ii.            Kuielekeza Sekretarieti kuweka mipango ya kuharakisha utekelezaji wa Mkakati huo; na

iii.          Kuridhia Sera ya Madini ya Kanda.

Ujumbe wa Tanzania uliridhia maazimio hayo, na kuchangia ajenda hii kwa kukifahamisha kikao kuhusu Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini na manufaa yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mfumo huo;

16. Mwongozo wa SADC wa ukusanyaji wa rasilimali

Mkutano ulipokea taarifa kutoka Sekretarieti ya SADC kuhusu rasimu ya Mfumo wa kutafuta fedha za kufadhili miradi ya maendeleo katika SADC (SADC Resource Mobilisation Framework). Mfumo huo umependekeza kwamba SADC ikusanye fedha za kufadhili miradi kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:

·         Mfuko wa Maendeleo wa Kanda;

·         Michango ya uanachama;

·         Mfumo wa kukusanya fedha kupitia kodi, tozo na harambee mbalimbali;

·         Michango ya ziara ya wanachama;

·         Michango kutoka sekta binafsi;

·         Michango kutoka taasisi za kiraia;

·         Michango kutoka kwa vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri; na

·         Ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Mfumo unaopendekezwa ulijadiliwa katika mkutano Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji katika mkutano uliofanyika mwezi Julai, 2019, Windhoek, Namibia ambapo Mawaziri waliridhia Mfumo huo wa kukusanya mapato kwa SADC, ambapo ilikubalika kila Nchi wanachama iwe huru kuchangia bajeti ya SADC kwa kutumia chanzo inachoona kinafaa bila kuathiri Uchumi wa nchi husik

Mkutano uliombwa kuridhia yafuatayo:

i.       Mfumo wa kutafuta fedha za kufadhili miradi ya maendeleo katika SADC (SADC Resource Mobilisation Framework) kwa mfumo unaoziruhusu kila Nchi Mwanachama kuchagua chanzo cha mapato katika kufadhili programu za kikanda na miradi (A La Carte), ikiwemo uwezekano wa kutumia rasilimali za ndani.

ii.      Miradi na programu itakayofadhiliwa lazima ibainishwe pamoja na mchanganuo wa bajeti na mahitaji ya michango kutoka Nchi Wanachama kwa kipindi ambacho mradi utatekelezwa kabla ya kupatiwa ufadhili.

Mapendekezo:-

Ø  Tanzania iliunga mkono azimio hili.

17.   UANZISHWAJI WA SADC VIRTUAL UNIVERSITY OF TRANSFORMATION

Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwezi Agosti, 2016  Eswatini, Mfalme Mswati III wa Eswatini aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2016 - Agosti 2017. Katika hotuba yake ya kufungua mkutano huo, Mfalme Mswati III alitangaza rasmi kuanzishwa rasmi kwa Chuo Kikuu cha Uhawilishaji cha SADC (SADC University of Transformation). Vilevile, Serikali ya Falme ya Eswatini iliomba kuwa makao makuu ya kiutawala ya chuo hicho na kuahidi kuwasilisha andiko kuhusu suala hili.

Chuo hicho kinalenga kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi (Technical – Vocational Educational Training) na teknolojia. Katika awamu ya kwanza ya mafunzo, chuo hicho kitatoa kipaumbele kwenye mafunzo yanayohusu sekta za madini, kilimo, madawa na uhandisi ili kuendana na mahitaji ya utekelezaji wa Mkakati wa Viwanda wa SADC (SADC Industrialisation Stratergy). Aidha, katika kutoa mafunzo hayo, chuo kinadhamiria kutumia vituo vya ufanisi (centres of excellence) vilivyopo katika vyuo vikuu vya Nchi Wanachama wa SADC.

Katika kutekeleza suala hili, Sekretarieti ya SADC imepata mshauri mwelekezi ambaye atafanya tathmini ya mahitaji ya ujuzi kwa upande wa SADC ambayo itasaidia katika kuandaa mitaala ya chuo hicho. Serikali ya Falme ya Eswatini imeombwa kukamilisha andiko kuhusu kuwa mwenyeji wa Ofisi ya Utawala ya Chuo Kikuu hicho na kuliwasilisha kwa mkutano wa Mawaziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia mwezi Juni, 2020.                                           

Hatimae Mkutano ulipokea taarifa ya utekelezaji wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Uhawilishaji cha SADC (SADC University of Transformation).

18.   KISWAHILI KUWA LUGHA RASMI YA NNE YA SADC (CONSIDERATION OF A PROPOSAL TO INTRODUCE KISWAHILI AS THE FOURTH SADC OFFICIAL LANGUAGE)

Katika mkutano huu, Lugha ya Kiswahili ilipitishwa rasmi na Wakuu wa Nchi na Serikali kutumika kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika.

Katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika mwezi Machi, 2019, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mhe. Palamagamba J.A.M. Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki uliwasilisha rasmi pendekezo la kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika SADC. Mpaka kufikia kipindi cha kufanyika mkutano huo, Jumuiya hii ilikuwa na lugha tatu ambazo ni Kireno, Kiingereza na Kifaransa.

Hivyo, katika mkutano huo, Tanzania ilifanikiwa kutumia fursa ya kuwa mwenyekiti wa SADC kusukuma suala hili na hatimaye kuwezesha Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi za SADC.

Andiko la kupendekeza matumizi ya Lugha ya Kiswahili liliandaliwa na Sekretarieti ya SADC, miongoni mwa masuala yaliyozungumziwa ni pamoja na historia ya lugha ya Kiswahili, matumizi yake hususan kama lugha iliyotumika wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika, kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili kama moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika na gharama za kuiongeza lugha hii. Aidha, andiko limeainisha pia sababu mbalimbali za msingi zilizolenga kuwavutia Nchi Wanachama kuunga mkono hoja hii.

Kulingana na tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya SADC, gharama za kuongeza lugha hii ambazo zinajumuisha matumizi ya watafsiri na wakalimani wakati wa mikutano ya SADC na gharama za kutafsiri nyaraka muhimu za kisheria za SADC zinakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani 245,200 kwa mwaka. Aidha, gharama za wakalimani pekee ni Dola za Kimarekani 88,400 kwa mwaka.

Katika mkutano wa Baraza la Mawaziri tarehe 14 Agosti, 2019, kufuatia majadiliano Tanzaina ilieleza kwamba itakuwa tayari kubeba gharama za wakalimani wa lugha ya Kiswahili kwa kipindi cha mwaka wa kwanza (Dola za Kimarekani 88,400). Hata hivyo, baada ya majadiliano kwenye mkutano huo, Nchi Wanachama zilikubaliana kuwa kwa vile azimio la kutumia lugha ya Kiswahili kwenye majadiliano limekubaliwa, si busara kuiachia Tanzania jukumu la kubeba gharama hiyo. Hivyo, Nchi Wanachama zikiongozwa na Jamhuri ya Botswana na Jamhuri ya Afrika Kusini zilikubaliana kwa pamoja kubeba gharama hiyo.

Sambamba na kupitishwa kwa kiswahili kuwa lugha rasmi ilikubalika kuwa kwa kuanzia lugha hiyo itatumika katika mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri.

19.         TAARIFA YA TATHMINI YA UTAYARI WA JAMHURI YA BURUNDI KUJIUNGA NA SADC

Kikao kilifahamishwa kuwa Jamhuri ya Burundi iliomba kujiunga na SADC. Mwezi Mei 2019 misheni maalum ya SADC ilitumwa nchini Burundi kufanya tathmini kulingana na vigezo vya kujiunga na Jumuiya hiyo. Misheni hiyo ilibaini kuwa sehemu kubwa ya vigezo hivyo vimetimizwa (70%). Aidha, misheni hiyo, ilibaini kuwa Burundi bado haijakidhi vigezo viwili ambavyo ni kutokuimarika kwa hali ya kiuchumi na hivyo kutilia shaka  uwezo wa nchi hiyo kutoa michango ya kila mwaka ya uanachama pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoafiki wazo la Burundi kujiunga na Jumuiya ya SADC. Hata hivyo, ni vema Burundi ikashughulikia kwanza changamoto zilizobainishwa na Misheni Maalum kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kujiunga na Jumuiya hiyo.

Mkutano ulipokea taarifa ya Burundi kuwa haijakidhi baadhi ya vigezo vya uanachama, na kuielekeza Sekretarieti ya SADC kuipatia Burundi taarifa ya tathmini hiyo, hususan maeneo yanayohitaji kuboreshwa kwa ajili ya utekelezaji kabla misheni nyingine ya uchunguzi haijatumwa nchini humo.

Mapendekezo :-

Ø  Tanzania iliunga mkono azimio hilo.

20. TAARIFA YA MSHIKAMANO WA SADC NA JAMHURI YA KIARABU YA SAHARAWI  MAGHARIBI (SADR)

20.1.    Taarifa ya Kongamano la Mshikamano wa SADC na Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi  Magharibi (SADR)

SADC iliona umuhimu wa kuonesha mshikamano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Saharawi Magharibi katika kuunga mkono ukombozi kamili katika bara la Afrika. Kwa muktadha huo, SADC iliandaa mkutano wa kikanda kwa ajili ya kuonesha mshikamano na Jamhuri ya Saharawi Magharibi uliofanyika tarehe 25 na 26 Machi, 2019, Pretoria, Afrika Kusini.

Kwa upande wa Tanzania, mkutano huo ulihudhuriwa na Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa Jumuiya za Kimataifa kuendelea kuunga mkono juhudi za kukomesha kukaliwa kimabavu kwa Jamhuri ya Saharawi na hivyo kuiwezesha kujitawala. Aidha, nchi za SADC zilikubaliana kuendelea kushikamana na Jamhuri ya Saharawi na pia kuendelea kuzungumzia suala hili katika mikutano ya kibara na kimataifa.

Mkutano uliombwa masuala yafuatayo:

i.             Kumpongeza Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake, na Jamhuri ya Afrika Kusini kwa kuandaa Kongamano hilo; na, uungwaji mkono wa Azimio la Kongamano hilo, hususan msimamo wa Umoja wa Afrika unaotaka Nchi zote Wanachama kualikwa na kushirikishwa katika Mikutano yote;

ii.            Kuzitaka Nchi Wanachama kuendelea kuunga mkono SADR, na kuendelea kupinga nchi zingine za bara la Afrika kukaliwa kimabavu; na,

iii.          Nchi Wanachama wa SADC kuunga mkono utekelezaji maazimio ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusu upatikanaji wa suluhu ya amani na ya kudumu inayokidhi matakwa ya watu wa Sahara ya Magharibi.

20.2.    Taarifa kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Saharawi Magharibi kuhusu ushiriki wao katika masuala ya Kibara na Kimataifa.

Mkutano ulitaarifiwa kuwa, mwezi Julai, 2019 SADR iliwasilisha andiko kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri  Mheshimiwa Netumbo Nandi – Ndaitwah kumtaarifu kuhusu nchi hiyo kutoalikwa kushiriki katika Mashindano ya Michezo mbalimbaliya Afrika yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2019 nchini Morocco; kutoalikwa katika Mkutano baina ya Japan na bara la Afrika (Tokyo International Conference on African Development- TICAD 7) ambao unatarajiwa kufanyika nchini Japan mwezi Agosti, 2019 pamoja na kutoalikwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Urusi na bara la Afrika (African – Russian Summit) unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2019 jijini Sochi, Urusi.

Mkutano uliombwa kuonesha mshikamano na SADR kwa kuhakikisha kuwa nchi hiyo inashirikishwa katika matukio hayo ya kibara na kimataifa.Tanzania iliunga mkono hoja hiyo

21.      KUBADILISHWA KWA JUKWAA LA BUNGE LA SADC KUWA BUNGE KAMILI LA SADC

Jukwaa la Bunge la SADC lilianzishwa mwaka 1997 kupitia makubaliano yaliyofanywa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC kwa mujibu wa Kifungu cha 9(2) cha Mkataba wa SADC kama Jukwaa la mashauriano ya Kibunge kuhusiana na masuala Kikanda. “Parliamentary Consultative Assembly for dialogue on issues of regional interest and concern”.

Lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hili ni kuwezesha Mabunge ya Nchi Wanachama kukutana na kufanya mashauriano yenye lengo la kuchochea kuwepo kwa sera za kikanda na pia kuweka mfumo utakaowezesha wananchi wa kawaida kutoa mchango wao kwenye sera za kikanda kupitia kwa wawakilishi wao. Pamoja na mambo mengine, Jukwaa hili limekuwa likitoa ushauri kwa Nchi Wanachama kwenye masuala mbalimbali ya kikanda pamoja na kuandaa sheria za mfano. Jukwaa hili linaendeshwa kupitia michango kutoka Nchi Wanachama na wafadhili mbalimbali. Nchi Wanachama huchangia Dola za Marekani 10,000 kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Jukwaa hilo.

Katika nyakati mbalimbali kuanzia mwaka 2004, 2008, 2011, 2015, 2018 na 2019 Jukwaa la Mabunge la Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika limekuwa likiwasilisha mapendekezo kuhusu kubadili Jukwaa hilo kuwa Bunge Kamili la SADC katika vikao mbalimbali vya SADC. Katika mkutano uliofanyika mwezi Agosti, 2018, Windhoek, Namibia, Wakuu wa Nchi na Serikali walipokea kwa mara nyingine tena pendekezo la kubadilisha Jukwaa la Wabunge wa SADC kuwa Bunge Kamili la SADC (Transformation of the SADC Parliamentary Forum into a SADC Parliament) ; na kuielekeza Sekretarieti ya SADC kukusanya maoni ya Nchi Wanachama kuhusu pendekezo hilo. Baadhi ya nchi ziliwasilisha maoni yao kuhusiana na mapendekezo hayo nchi hizo ni Angola, Mauritius, Eswatini, Msumbiji, Seychelles, Afrika Kusini na Zambia.

Kwa upande wa Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha Tisa cha Mwaka 2008, lilipitisha Azimio Na. 30/2018 linalojulikana kama Azimio la Bunge la kuunga mkono kuanzishwa kwa Bunge la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Establishment of a SADC Parliament).  Mwezi Machi, 2019, Bunge la Tanzania liliwasilisha tena msimamo wake wa kuunga mkono kuanzishwa Bunge la SADC na kueleza kwamba hatua hiyo itaongeza msukumo wa utekelezaji wa masuala ya SADC na itawezesha ulinganifu wa sheria (harmonization) baina ya Sheria zinazotungwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile za SADC; na hivyo kupunguza migongano baina ya sheria zinazotungwa na Nchi Wanachama wa SADC.

Mapema mwezi Machi, 2019 pendekezo hili lilipotolewa tena kwenye Mkutano wa Mawaziri wa nchi za SADC uliofanyika Jijini Windhoek, Namibia, Mawaziri hao walielekeza kwamba kiundwe kikosi kazi cha Asasi Mbili za Utatu wa SADC (SADC Double Troika Task Force) kitakachoshirikisha nchi sita ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Namibia, Tanzania, Zambia, na Zimbabwe, Sekretarieti ya SADC na Sekretarieti ya SADC PF. Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge, Sera na Uratibu ilishiriki kikosi kazi hicho.

Katika kufanyia kazi suala hili, kikosi kazi hicho kilielekezwa kufanya tathmini ya kina kuhusiana na masuala yafuatayo: mamlaka ya Mabunge ya kikanda, mfumo wa kisheria, muundo na majukumu ya Mabunge hayo, mahusiano baina ya Taasisi na Mabunge ya Kikanda,  mahusiano ya Mabunge ndani na nje, wajibu wa Mabunge ya kikanda kwa sheria za kimataifa na masuala ya upatikanaji wa fedha, gharama na mfumo wa uchangiaji. Aidha, Kikosi kazi hicho kilifanya ziara katika Bunge la Afrika, Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, Bunge la Ulaya na Bunge la Asia ili kufahamu utendaji wa Mabunge hayo na kuishauri Jumuiya ya SADC ipasavyo. Mkutano huu ulitaarifiwa kuwa taarifa ya Kikosi kazi cha SADC Double Troika imekamilika.

Mkutano uliombwa kupokea taarifa kwamba Sekretarieti ya SADC na Jukwaa la Wabunge wa SADC zitafanya tathmini ya kina kuhusu muundo unaopendekezwa kwa Bunge la SADC, zitatengeneza mpango-kazi wa kubadilishwa kwa Jukwaa la SADC kuwa Bunge la SADC, na zitawasilisha taarifa kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali mwezi Agosti, 2020.Tanzania iliunga mkono hoja hiyo.

22. KUUNGA MKONO ZIMBABWE KUONDOLEWA VIKWAZO VYA KIUCHUMI

Mkutano huu utafahamishwa kuwa, mkutano Mawaziri wa Kisekta wenye dhamana ya masuala ya Jinsia na Wanawake uliofanyika mwezi mei, 2019 Windhoek Namibia, pamoja na mambo mengine, ulibainisha hali ya uwepo wa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani pamoja na washirika wake nchini Zimbabwe. Hali hii imeathiri maendeleo ya kiuchumi nchini humo pamoja na hali ya maisha ya wananchi ikiwemo makundi maalum ya wazee, watu wanaoishi na ulemavu pamoja na watoto). Kwa muktadha huu, hali hiyo imeathiri maendeleo ya kiuchumi ya wanawake pamoja na kuwepo athari za kikanda. Hali hiyo inalazimu kuwepo kwa jitihada za kikanda kukabiliana na vikwazo hivyo.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika mwezi Agosti, 2019 Dar es Salaam na Mkutano wa 797 wa Mkutano wa Mawaziri wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika Septemba, 2018, ilitaka vikwazo dhidi ya Zimbabwe viondelewe ili kuwezesha uchumi wa nchi hiyo kuimarika. Serikali ya Zimbabwe pia itawasilisha taarifa kuhusu athari za vikwazo hivyo kwa makundi mbalimbali nchini humo, ikiwemo wanawake, watoto na wazee.

Mkutano huo uliombwa masuala yafuatayo:

i.   Kuridhia Mwenyekiti wa SADC kuwasilisha msimamo rasmi wa SADC unaotaka vikwazo dhidi ya Zimbabwe viondolewe katika hotuba yake kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kuwaasa Wakuu wa Nchi na Serikali wengine kuweka suala hilo kwenye hotuba zao kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa;

ii.  Kuridhia tarehe 25 Oktoba, 2019 kuwa siku rasmi kwa Nchi Wanachama wa SADC kuelezea kupinga vikwazo hivyo kwa kupitia shughuli mbalimbali;

iii. Kufanya mashauriano na nchi zilizoweka vikwazo dhidi ya Zimbabwe  ikiwemo kupitia Kundi la Mabalozi wa SADC katika nchi mbalimbali;

iv. Kuielekeza Sekretarieti ya SADC kuhakikisha kwamba suala la kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Zimbabwe linajumuishwa kwenye ajenda za majadiliano na wabia wa kimataifa wa maendeleo, na kutengeneza mpango wa kuimarisha uratibu wa mashauriano na nchi ambazo zinaweka vikwazo dhidi ya Nchi Wanachama wa SADC.

Mapendekezo

Ø  Tanzania iliunga mkono hoja hiyo

23.           MAKUBALIANO NA MIKATABA INAYOPENDEKEZWA KUSAINIWA

a)            Uwekaji saini na Uridhiaji wa Itifaki za SADC

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inajumla ya Itifaki 30 katika Kanda. Mkutano huu ulipokea taarifa ya Itifaki ambazo zimeshaanza kufanya kazi na zile ambazo bado hazijaanza kufanya kazi. Utaratibu wa SADC ni kwamba Itifaki inaanza kufanya kazi baada ya kuridhiwa na theluthi mbili (2/3) ya Nchi Wanachama.

Hadi kufikia mwezi Julai, 2019 Tanzania imeshasaini jumla ya Itifaki 29 na Makubaliano 18. Kati ya Itifaki hizo, Itifaki 23 zimesharidhiwa (ratified) na Itifaki 6 ziko katika hatua mbalimbali za kuridhiwa. (Orodha ya Itifaki hizo imeambatishwa) kwa urahisi wa rejea.

Mkutano utaombwa kuzisisitiza nchi ambazo hazijasaini na kuridhia Itifaki za SADC zifanye hivyo mapema na kuwasilisha nyaraka za uridhiaji kwenye Sekretarieti ya SADC ili Itifaki hizo ziweze kuanza kutekelezwa.

Mapendekezo ya msimamo wa Tanzania

Ø  Tanzania iliunga mkono azimio hilo.

b)   Rasimu ya Itifaki ya Msaada wa Kisheria katika Kesi za Jinai

Mkutano huu ulipokea taarifa kuwa, Mkutano wa Mawaziri wa Sheria na Wanasheria Wakuu wa Serikali na wa Jumuiya ya SADC uliofanyika mwezi Agosti, 2019 ulifanyia marekebisho kipengele namba 9 cha itifaki ya msaada wa kisheria inayohusu kuthibitisha uhalali wa nyaraka.

Aidha, mapendekezo hayo yatawasilishwa katika mkutano huu ili Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC waweze kuridhia marekebisho hayo.

c)    Rasimu ya Mkataba wa Kuboresha Kifungu Na. 7 (1) cha Taratibu za kuhakiki nyaraka ndani ya Itifaki ya Kubadilishana Wahalifu (Draft Agreement Amending Article 7 (Authentication of Documents) of the Protocol on Extradition

Mkutano utaombwa kurejea Kifungu Na, 7 (1) cha Itifaki ya Kubadilishana Wahalifu ambacho kinazungumzia uhakiki wa nyaraka kulingana na Sheria za nchi zinazowasilisha maombi. Hata hivyo, imeonekana kuwa sheria za uhakiki wa nyaraka za nchi zinaongozwa na sheria za nchi iliyoombwa na sio nchi iliyoomba; na sababu ya msingi kutumia sheria ya nchi iliyoombwa ni kurahisisha taratibu za kupokea na kutumia nyaraka katika vyombo vya sheria.

Kamati ya Mawaziri wa Sheria na Wanasheria Wakuu katika mkutano uliofanyika mwezi Machi, 2019, Windhoek, Namibia walijadili maboresho yanayopendekezwa na kuridhia yawasilishwe kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi.

Mkutano utaombwa kuridhia maboresho ya Kifungu Na. 7 (1) cha Itifaki ya Kubadilishana Wahalifu kinachohusu taratibu za kuhakiki nyaraka ili nyaraka hizo ziweze kuhakikiwa kulingana na sheria na taratibu za nchi iliyoombwa kubadilishana wahalifu. Tanzania iliunga mkono azimio hilo.

d)   Uteuzi wa Majaji wa Mahakama wa SADC (Re-Appointment of SADC Administrative Tribunal (SADCAT) Judges)

SADC Adminisrative Tribunal - SADCAT ni Mahakama ya SADC inayohusika na kutafsiri Mkataba wa SADC pamoja na sheria nyingine za SADC ikiwemo Sheria zinazoongoza masuala ya usimamizi wa rasilimali watu kwenye SADC. Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2005 na makao makuu yake yapo Windhoek, Namibia.

Mahakama hiyo inaongozwa na Majaji saba (7) ambao wanachaguliwa kutoka kwenye Nchi Wanachama na wanatumikia nafasi hizo kwa kipindi cha miaka miwili. Jaji Regina Rweyemamu ni Mtanzania ambaye ni miongoni mwa majaji 7 wanaohudumu katika mahakama hiyo.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika mwezi Machi, 2019 uliridhia Majaji wa Mahakama hiyo kuongezewa muda. Aidha, uliielekeza Sekretarieti ya SADC kuanza mchakato wa kufanya mabadiliko ya Mkataba unaoanzisha Mahakama hiyo (Article V (5) of the SADCAT Statute) ili kuruhusu majaji hao kumaliza muda wao kwa awamu badala ya wote kumaliza kwa wakati mmoja jambo ambalo linapelekea kupoteza mwendelezo wa masuala yanayofanyiwa kazi kwenye mahakama hiyo. Rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo imekamilika.

Mkutano uliombwa kuridhia mabadiliko ya Sheria ya Mahakama ya SADC (SADCAT Statue) kwa ajili ya utekelezaji.

Mapendekezo

Ø  Tanzania iliunga mkono azimio hili

e)    Itifaki ya  Uhamishaji wa Wahalifu waliohukumiwa katika Nchi Mwanachama wa SADC

Itifaki hii inahusu uhamishaji wa wahalifu waliohukumiwa kutumikia vifungo vyao katika nchi zao ili waweze kutoa mchango wa kijamii kama raia ambao wamehukumiwa kwa sababu ya makosa ya jinai waliyoyafanya katika nchi za kigeni. Itifaki hii  imeandaliwa kama sehemu ya ushirikiano wa SADC katika masuala ya  sheria na haki na ni moja wapo ya masuala yaliyopendekezwa katika Mpango wa Utendaji wa Kamati ya Mawaziri wa Sheria / Mawakili Mkuu iliyopitishwa katika mkutano wake uliofanyika jijini Gaborone, Botswana Julai 2016.

Baraza la Mawaziri katika mkutano uliofanyika Lusaka, Zambia Julai, 2019, walijadili Itifaki hii na kuridhia iwasilishwe katika Kamati ya Mawaziri wa Sheria na Wanasheria Wakuu kwa ajili ya uhakiki (legal clearance) na hatimaye iwasilishwe katika Baraza la Mawaziri kwa uamuzi.

Kamati ya Mawaziri wa Sheria na Wanasheria Wakuu katika mkutano uliofanyika Swakopmund, Namibia mwezi Agosti, 2019 walijadili Itifaki hii na kuridhia iwasilishwe kwa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa ajili ya kuridhia na kusaini.

Mkutano uliombwa kupokea na kuridhia Itifaki ya Uhamishaji wa Wahalifu kwa Nchi Wanachama wa SADC

    Mapendekezo

Ø    Tanzania iliunga mkono azimio hili

24.   NCHI MWENYEJI NA TAREHE YA KUFANYIKA KWA MKUTANO UJAO

Mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa mwaka 2020 utafanyika Maputo, Jamhuri ya Msumbiji kwa tarehe itakayopangwa na nchi mwenyeji kwa kushirikiana na sekretarieti ya SADC.

25. TAARIFA KWA UMMA (COMMUNIQUÉ)

Baada ya kukamilika kwa mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, tamko la mkutano huo lilitolewa rasmi kwa Umma tarehe 18 Agosti, 2019 katika kilele cha kuhitimisha mkutano huo.

26.   HITIMISHO

Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ulihitimishwa kwa kutolewa Tamko la Mkutano ambalo lilitoa taarifa fupi kuhusu masuala yaliyojadiliwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwa ufahamu w

  • Google+
  • PrintFriendly